

Na mwandishi wetu
Uhalifu Mtandaoni
Katika ulimwengu wa teknolojia unaokua kwa kasi, uhalifu wa mtandaoni umeibuka kwa mbinu mpya zinazotumia vifaa vya watu bila wao kujua. Moja ya mbinu hizo ni kile kinachojulikana kama Botnet, mtandao wa siri wa kompyuta, simu au server zilizoambukizwa na programu hatari (malware) na kudhibitiwa na wahalifu kutoka mbali.
Jinsi Botnet Inavyoundwa.
Kwa kawaida, mhalifu huanza kwa kusambaza programu hatari kupitia njia mbalimbali kama barua pepe za ulaghai (spam), link bandia, tovuti zenye virusi au kupitia upakuaji wa programu zisizo salama. Mtumiaji akifungua link au kupakua faili hiyo, kifaa chake kinaweza kuambukizwa bila yeye kutambua.
Baada ya kuambukizwa, kifaa hicho huanza kufanya kazi chini ya udhibiti wa mhalifu. Mara nyingi mmiliki wa kifaa hagundui chochote kinachoendelea. Katika ulimwengu wa usalama wa mtandao, vifaa hivyo huitwa “zombie computers” au “zombie phones” kwa sababu vinafanya kazi kwa amri ya mtu mwingine bila mmiliki kujua.
Mfumo wa Udhibiti wa Botnet
Botnet nyingi hudhibitiwa kupitia kitu kinachoitwa Command and Control Server (C&C). Hiki ni kituo cha udhibiti ambacho hutumiwa na mhalifu kutuma maagizo kwa maelfu au hata mamilioni ya vifaa vilivyoambukizwa duniani kote. Kupitia mfumo huo, wahalifu wanaweza kuamuru vifaa hivyo kufanya shughuli mbalimbali kwa wakati mmoja.
Botnet Hutumika Kufanya Nini?
Wahalifu hutumia botnet kwa malengo kadhaa ya uhalifu wa mtandaoni. Mojawapo ni kutuma spam, ambapo maelfu ya kompyuta au simu hutuma barua pepe au ujumbe wa ulaghai kwa watu wengi kwa wakati mmoja.
Pia botnet hutumika kusambaza virusi vipya kwa watumiaji wengine wa mtandao, jambo linaloongeza idadi ya vifaa vilivyoambukizwa. Aidha, botnet hutumiwa kufanya mashambulizi ya mtandao yanayojulikana kama Distributed Denial of Service (DDoS). Katika mashambulizi hayo, maelfu ya vifaa hutuma maombi mengi kwa website moja hadi mfumo wake ushindwe kufanya kazi.
Mbali na hayo, baadhi ya botnet hutumika kuiba taarifa za siri kama passwords, taarifa za benki au kufuatilia shughuli za mtumiaji kwenye mtandao.
Mfano wa Botnet Kubwa Duniani
Katika historia ya uhalifu wa mtandao, botnet mojawapo iliyowahi kuwa hatari ni GameOver Zeus, ambayo ilitumika kuiba mamilioni ya dola kupitia wizi wa taarifa za benki za watumiaji wa mtandao.
Dalili Kifaa Chako Kinaweza Kuwa Kimeambukizwa
Wataalamu wa usalama wa mtandao wanaeleza kuwa dalili kadhaa zinaweza kuonyesha kifaa kimeambukizwa. Miongoni mwa dalili hizo ni pamoja na internet kuwa polepole bila sababu, matumizi makubwa ya data yasiyoeleweka, au kuonekana kwa programu ambazo mtumiaji hakuzipakua.
Namna ya Kujilinda
Ili kujilinda dhidi ya hatari ya botnet, wataalamu wanashauri watumiaji kuepuka kupakua programu kutoka vyanzo visivyo rasmi, kutumia programu za usalama na kufanya masasisho ya mara kwa mara ya mfumo wa simu au kompyuta. Pia ni muhimu kuepuka kufungua link zisizoaminika zinazotumwa kupitia SMS au barua pepe.
Kwa ujumla, kadri matumizi ya teknolojia yanavyozidi kuongezeka, ndivyo umuhimu wa kuwa makini na usalama wa mtandao unavyoongezeka. Botnet ni mfano wa wazi wa jinsi vifaa vya kawaida vinaweza kugeuzwa zana ya uhalifu bila mmiliki kujua.
