

Afisa wa ofisi ya wakala wa vipimo mkoa wa Shinyanga, Leo Patrick akitoa elimu katika kituo cha uzaji wa mafuta kwa vyombo vya usafiri juu ya umuhimu wa kutambua vipimo katika kuadhimisha siku ya vipimo duniani.
Na Kareny Masasy,
Shinyanga
WAKALA wa Vipimo mkoa wa Shinyanga (WMA) umetoa elimu kwa baadhi ya waendesha bodaboda kwaajili ya kuthibiti Vipimo kwenye vituo vya utolea huduma ya mafuta ili kujua hali halisi ya Vipimo wanavyovipata kama ni sahihi.
Hayo yamesemwa leo mei 19,2025 na Ofisa Vipimo, Leo Patrick katika kuadhimisha siku ya vipimo duniani iliyoendana na utowaji wa elimu na namna ya kutambuzi wa pampu yenye stika ya Wakala ya Vipimo iliyothibitishwa kwa matumizi halali ya utoaji huduma na yenye kipimo halali.
Patrick amesema kauli mbiu ya mwaka huu ni vipimo kwa Watu wote na Muda wote ikiwa utoaji wa elimu hii lengo lake ni kubaini pampu hizo kama zinatumika kwa kuendana na uhalisi wa Vipimo kama inavyohitajika.
“Elimu leo tumeitoa ili kuweza kuthibiti wimbi la wizi kwa watumiaji kwani dhima ya Wakala wa Vipimo ni kuhakikisha mlaji au mtumiaji anakuwa kwenye hali ya Usalama,afya,kibiashara na Mazingira” amesema Patrick.
Patrick amesema utoaji wa elimu kwenye vituo vya mafuta ni moja ya eneo linalohusika na Wakala wa Vipimo kwa kuthibitisha kuwa Vipimo ni sahihi ikiwa maeneo mengi wamekuwa wakihusika katika kutoa elimu na kuthibiti kupunja walaji.
Ofisa Vipimo Baraka Mbizo amesema leo ni siku ya vipimo duniani na wametembelea kituo cha mafuta na kuna stika iliyopo kwenye mashine inaonyesha ilikaguliwa lini na mwisho wa matumizi ya pampu ni lini.
Mbizo amesema muda wowote wamekuwa wakifanya ukaguzi wa kushtukiza na wamekuwa wakitoa elimu mara kwa mara na kuhakikisha pampu inakuwa inaanzia namba sifuri bila kuingiliana na mteja mwingine.
Mbizo amesema pindi wakipata malalamiko kuwa kituo fulani kinafanya udanganyifu na uchunguzi ukafanyika na kubainika kuwa kweli hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za Wakala wa Vipimo za mwaka 2002 kwa kutozwa faini .
Mbizo amesema faini hizo zinazotozwa kwa mujibu wa sheria pindi mmiliki akikutwa na makosa ambapo itatozwa shilingi milioni 3 hadi tano au kifungo cha miaka mitatu kwenda jela.
Mwenyekiti wa kituo cha bodaboda mtaa wa ushirika,Frank Mahende alipongeza wakala wa vipimo kwa elimu waliyoitoa kujua stika iliyowekwa ina umuhimu wa kujua uhalali wa vipimo kwenye mafuta wanaoupata kutokana na safari wanazozunguka.
Mwendesha bodaboda Hamis Mshandete mkazi wa ushirika manispaa ya Shinyanga amesema Wakala wa Vipimo wametoa elimu na amejifunza namna ya uwepo wa stika zilizo kwenye mashine ili kuweza kupata mafuta kupitia Vipimo halali.



